Na Valentine Oforo
DODOMA. ZAIDI ya watoto 50 wanaocheza mchezo wa Tenisi wameshiriki katika Mashindano ya Pili ya Katoto Tenisi yaliyofanyika jana katika Jiji la Dodoma.
Mashindano hayo yaliyoandaliwa na Kituo Cha Kutoa Mafunzo ya Tenisi Cha Katoto (Katoto Tennis Academy) kilochopo Jijini Dodoma yaliwashirikisha wachezaji wachanga wa Tenisi Kutoka Mikoa ya Arusha, Dar es Salaam, Morogoro na Wenyeji Dodoma.
Akiongea na Waandishi wa Habari kando ya Mashindano hayo, Bwn Paul Ngavi, Mratibu wa Mashindano hayo ambaye pia ni Kocha Mkuu wa Kituo Cha Tenisi Cha Katoto amesema lengo la kuanziaha Mashindano hayo ni kukuza mchezo wa Tenisi katika Mkoa wa Dodoma, na Kanda ya Kati kwa ujumla.
"Wakati tunaanzisha hiki kituo, tulianza na watoto wanne tu waliokuwa wakipatiwa mafunzo, lakini leo tunafurahi kwamba tuna zaidi ya wanafunzi 40 wanaojifunza Tenisi hapa," alisema.
Mtaalam huyo Nguli wa Tenisi Kutoka Nairobi, Kenya alisema kituo kina mipango mingi ya kimkakati ya kukuza mchezo wa Tenisi Jijini Dodoma.
Mikakati hiyo, pamoja na mingine ni kuanzisha vilabu maalumu vya kutoa mafunzo ya mchezo huo kuanzia ngazi ya chini, ikiwa ni pamoja na katika shule za awali na msingi.
Aidha, alitoa wito kwa Serikali kuunga mkono Mpango wa kuanzisha vilabu vya Tenisi katika ngazi za awali.
Kwa upande wake, Bwn Bernald Konga, Baba wa Noran Konga, mwanafunzi anayeshiriki mchezo wa Tenisi katika kituo hicho alitoa wito kwa wazazi kuwawezesha watoto wao kujiunga na Kituo Cha Tenisi Cha Katoto.
"Katika maisha yangu nimekuwa nikicheza michezo mbalimbali ikiwemo soka, mpira wa mkono na mpira wa kikapu, lakini sikuwahi kufikiria Tenisi,"
"Kwa hivyo ilipofika wakati wa kuchagua mchezo ambao nilitaka kumsaidia binti yangu kujifunza wazo la mchezo wa Tenisi likanijia, haswa baada ya kukifahamu Chuo cha Tenisi ya Katoto," alisema.
Bwn Konga alisema tangu mtoto wake ajiunge na mchezo wa Tenisi, amedhihirisha ukuaji mzuri wa afya ya mwili na akili.
Mzazi mwingine, Bi Sharifa Adon kutoka Arusha alizungumza juu ya hitaji la wazazi, na jamii kwa kubwa kuondokana na fikra potofu kwamba mchezo wa Tenisi ni kwa ajili ya matajiri pekee.
"Kwa mfano, katika Chuo cha Tenisi ya Katoto kuna watoto wengine ambao wametoka katika vituo vya kuwalea watoto yatima, na kwenye familia duni," alisema.
Hellen Mtaka, mchezaji mchanga wa Tenisi kwenye Chuo Cha Katoto kwa upande wake alisema: "Nilianza mafunzo ya Tenisi katika kilabu hiki nikiwa na umri wa miaka mitatu, na hadi sasa nimeweza kujifunza na kuuelewa mchezo kwa kiasi cha kushindana na kushinda kwenye mashindano tofauti maarufu nchini,"
Aliongeza, mchezo wa Tenisi ni muhimu katika kuburudisha akili, lakini pia husaidia mchezaji kuongeza uwezo wa kufanya maamuzi kwa wakati, pamoja na uelewa na ufaulu katika masomo.
Post a Comment