👉 Mahitaji Halisi Ya Mbegu Bora Nchini Kwa Sasa Ni Tani 127,650 Kwa Mwaka, Wakati Utoshelevu Ni Tani 70,000
MOROGORO. WAKALA Wa Mbegu Za Serikali (ASA) inafanya kazi kuongeza wigo wa uzalishaji wa mbegu bora nchini kwa kiwango cha kufikia tani 22, 344 katika msimu ujao wa kilimo wa 2025/26.
Katika msimu wa kilimo wa 2024/25, ASA ilizalisha jumla ya tani 9,303 za mbegu bora za mazao mbalimbali ya kimkakati, kiasi ambacho ni ongezeko la asilimia 106.27 ya mbegu zilizozalishwa wakati wa msimu wa 2023/24, tani 4,510.
Mkurugenzi Mkuu Mtendaji (CEO) wa ASA, Bwn Leo Mavika ameiambia 'SwahiliNewz' wakati wa mahojiano maalumu kuwa Wakala umeshuhidia ongezeko kubwa katika uzalishaji wa mbegu tangu kuanza kuingia mikataba na wazalishaji wa mbegu toka sekta binafsi.
"
Kwa kiwango kikubwa, wazalisha mbegu wa mikataba wamefanya, na wanaendelea kufanya kazi kubwa katika kuiwezesha ASA kuongeza wigo wake wa uzalishaji wa mbegu," Bwn Mavika alieleza.
Aliongeza kuwa, Wakala umeingia mikataba na takribani wazalisha mbegu 102 ambao kwa sasa wanaendelea kizalisha mbegu bora katika mashamba mbalimbali yanayomilikiwa na Serikali.
"Mahitaji halisi ya mbegu bora nchini kwa sasa ni tani 127,650 kwa mwaka, wakati utoshelevu wa mbegu ni tani 70,000," Mkurugenzi alisema.
Bwn Mavika ameongeza kuwa, katika mwaka huu wa fedha, Serikali imeipatia ASA kiasi cha Shilingi Bilioni 51, kiasi ambacho kitatumika kwa ajili ya kuiwezesha Wakala kutekeleza na kukamilisha mikakati ya kuboresha na kuongeza uzalishaji wa mbegu nchini.
ASA, yenye Makao yake Makuu Mkoani Morogoro, kwa sasa inamiliki jumla ya hekari 17,000 za ardhi kwa ajili ya uzalishaji wa mbegu.
Hata hivyo, kati ya hekari hizo, ni hekari 13,600 tu ndizo zinazotumika kwa ajili ya uzalishaji wa mbegu nchini.
Katika kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabia nchi yanayotajwa kuathiri sekta ya kilimo kwa kiasi kikubwa hapa nchini, Wakala umejikita katika mradi mkubwa wa ufungaji wa miundombinu ya kisasa ya umwagiliaji katika mashamba yake ya uzalishaji mbegu.
Mpaka sasa, Bwn Mavika anasema ASA imefaninikwa kufunga miundombinu hiyo katika mashamba kadhaa, ikiwemo shamba la Kilimi, Arusha and Msimba.
"Miradi ya ufungaji wa miundombinu ya kisasa ya umwagiliaji itafungwa katika mashamba yetu yote nchini, hivi karibuni ufungaji utaanza kwenye mashamba ya Namtumbo, Mbozi na Mwele," Ameeleza.
Post a Comment