DIWANI RINGO AFICHUA SIRI ZA KUIJENGA KATA YA MIYUJI UPYA



"Mimi Ni Mpole, Mkarimu na Mnyenyekevu, Ila Siyo Mnyonge Linapokuja Swala La Maendeleo," Diwani Ringo


DODOMA. DIWANI Mteule wa Kata ya Miyuji Jijini Dodoma kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM,) Bwn Ringo Iringo amesema ameandaa Mkakati Kabambe (MK) wa kuijenga Kata hiyo upya na kuboresha maisha ya wakazi wake.

Akizungunza wakati wa mkutano maalumu wa kuzindua rasmi kampeni yake uliyofanyika katika viwanja maarufu vya abiria katika Kata hiyo, Ringo alisema utekelezaji wa mkakati huo unaoakisi ilani ya CCM utashuhudia mapinduzi makubwa katika sekta mbalimbali.

Sekta hizo, alisema ni pamoja na Elimu, Upatikanaji wa Maji Safi na Salama, Afya, Uboreshaji wa Miundombinu ya Barbara, Uwezeshaji Wananchi Kiuchuni, pamoja na huduma kwa walemavu na wazee.

"Mimi ni mpole, mkarimu na mnyenyekevu, Ila siyo mnyonge linapokuja swala la maendeleo," Bwn Ringo alisema.

Ringo, ambaye anajinadi kwa kauli mbiu ya ' Tupo Site Tunajenga Miyuji Mpya', ameitaja baadhi ya mikakati atakayoitekekeza kuwa ni pamoja na ujenzi wa miundombinu ya barabara kwenye maeneo muhimu yenye uitaji, kwa viwango vya lami na changarawe.

" Ndugu zangu ukitembea Jijini Dodoma utagundua Kata ya Miyuji ndiyo Kata ambayo iko nyuma sana kimaendeleo, hivyo nataka kuifungua Miyuji kimaendeleo kwa kuboresha miundombinu ya barabara," Diwani Ringo alieleza.

Amezitaja baadhi ya barabara muhimu ambazo atahakikisha zinajengwa kwa kiwango cha lami kuwa ni zile za kutoka Upendo hadi Mpamaa, na kutoka Chuo Cha Mipango hadi Mpamaa.

"Barabara hizi ni muhimu sana katika kuchochea ukuaji wa uchumi katika Kata ya Miyuji, hivyo nitahakikisha zinajengwa kwa kiwango cha lami na kufungwa taa za kisasa," Diwani Ringo alisisitiza.

Eneo jingine muhimu ambalo ameahidi kulitendea kazi ni Elimu, ambapo alisema atahakikisha shule ya Sekondari ya kisasa inajengwa katika Kata ya Miyuji.

"Kwa miaka mingi sasa watoto wetu wamekuwa wakilazimika kutembea umbali mrefu kwa ajili ya kutokuwepo kwa shule ya Sekondari katika Kata yetu, hiki nitalimaliza," Bwn Ringo aliahidi.

Pamoja na hatua hiyo, Diwani Ringo ameahidi kujenga vyumba zaidi vya madarasa katika shule za msingi za Mpamaa na Mlimwa 'C' ambapo kuna upungufu mkubwa vya miundombinu hiyo muhimu ya kusomea.

Aidha, changamoto ya upungufu mkubwa wa nyumba za waalimu katika Kaya ya Miyuji ni eneo jingine nyeti ambalo Diwani Ringo ameahidi kulipatia ufumbuzi.

Akizungunza kuhusu kuwawezesha Wananchi Kiuchuni, Ringo amesema atahakikisha Vijana, Wanawake na Walemavu wananufaika ipasavyo na mikopo inayotolewa na Serikali kupitia Halmashauri.

"Nina uzoefu wa kutosha katika maswala ya kuandika Mipango ya biashara, hivyo, pamoja na kuwasaidia Wananchi wangu kunufaika ni mikopo hiyo, nitajitolea muda na uzoefu wangu kuwasaidia ili waweze kuandika mipango rafiki ya biashara, na namna ya kuhakikisha wanafanya biashara kwa ufanisi na kwa viwango vitakavyowawezesha kurejesha mikopo hiyo kama Sheria husika inavyoelekeza," aliahidi.

Akieleza zaidi, Diwani Ringo ameahidi kufungua Kongani la viwanda katika Kata ya Miyuji Ili kuwapa fursa Wananchi kujikita katika kuanzisha viwanda vidogo na vile vya kati vitakavyokuwa vikichakata bidhaa mbalimbali.

"Pia, nitasimama mstari wa mbele kuhakikisha Wananchi wenye vipaji na bunifi mbalimbali wanashikwa mkono Ili kutimiza ndoto zao," aliongeza.

Ringo alitumia mkutano huo kuwahamasisha Wananchi kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura Ili waweze kutumia haki yao ya kikatiba ya kupiga kura.

"Nawaombeni sana mumpe kura za ndiyo Mgombea wa kiti cha Uraisi kwa tiketi ya CCM, Mh. Dkt Samia Suluhu Hassan Ili aweze kuendeleza kazi njema za kuijenga Tanzania," alisema.


Post a Comment

Previous Post Next Post