WIZARA YA MALIASILI NA UTALII KWENYE MKAKATI KUVIPA VITUO VYA UTALII DODOMA HADHI YA KIMATAIFA

 



                             Bwn. Mathew Kiondo


👉 Wawekezaji Wakaribishwa Kujenga Hoteli Za Nyota Tano Kwenye Vituo

👉 Serikali Kuboresha Huduma, Bidhaa Za Kitalii Kwenye Vituo Vya Utalii Dodoma

Vituo Husika Ni Pamoja Na Kituo Cha Michoro Ya Kale Kondoa Irangi, Mapori Ya Akiba Ya SwagaSwaga Na Mkungureno 


DODOMA. SERIKALI, kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imeanza kutekeleza mkakati maalumu  wa kukuza vituo vyote vya Utalii vinavyopatikana Mkoani  Dodoma, na Kanda ya kati kwa ujumla.

Mkakati huo, unalenga kuboresha miundombinu na hadhi ya vituo vya Utalii vya Mapori ya akiba ya Mkungunero na SwagaSwaga, pamoja Kituo cha michoro ya kale ya miambani cha Irangi, kilichopo eneo la Kolo, Wilayani Kondoa, Mkoani Dodoma.

Akizungumza wakati wa ziara maalumu ya kitalii katika kituo cha michoro ya miambani cha Kondoa Irangi, Kaimu Mkurugenzi wa Sehemu ya Uendelezaji wa Utalii, Idara ya Utalii, Wizara ya Maliasili na Utalii, Bi. Dainess Kunzugala amesema Wizara inatekeleza Mkakati huo kwa ushirikiano na Wakala Wa Misitu Tanzania (TFS), Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), pamoja na wadau kutoka sekta binafsi.


 Bi. Dainess Kunzugala


Pamoja na mambo mengine, amesema mkakati huo endelevu pia unalenga kuhakikisha vituo hivyo vinafikia viwango vya kimataifa, haswa kuwa na vigezo muhimu vitano vinavyotakiwa.

Vigezo hivi ni pamoja na kuhakikisha vituo vinakuwa na miundombinu mizuri ya barabara Ili kufikia kwa urahisi, vifaa vyote muhimu vya utalii, hoteli  za kisasa za kuanzia nyota tatu na tano, huduma zote muhimu za kijamii, pamoja na bidhaa nyingi zaidi za kitalii, ikiwemo sehemu maalumu za michezo mbalimbali, pamoja na sehemu za michezo ya watoto," alieleza.


Ziara hiyo, ambayo iliratibiwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma kwa ushirikiano na Kampuni ya Epic Adventures, TTB na TFS, ilifanyika Septemba 27, 2025 kwa jina la " Nyama Choma Bata Pori' kwa lengo la kuadhimisha siku ya Utalii Duniani.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kampuni ya Epic  Adventures, Bwn. Joel William amesema licha ya kuadhimisha siku ya Utalii Duniani, Kampuni yake imeamua kuandaa ziara hiyo kwa lengo la kusaidia jitihada za kukuza sekta ya utalii kanda ya kati.

"Tumeamua kuandaa ziara hii ya kitalii kwa ajili ya kuunga mkono jitihada mbalimbali zinazotekelezwa na Raisi Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kukuza sekta ya Utalii nchini," alisema.

Amesema Dodoma imebarikiwa kuwa na vivutio vizuri vya Utalii ambavyo vinahitaji jitihada jumuishi kutoka serikalini na sekta binafsi Ili kuvitangaza na kuviboresha.

"Tumejipanga kuandaa safari, pamoja na matukio mbalimbali kwa lengo la kuhakikisha sekta ya Utalii Mkoani Dodoma inakuwa kwa kasi kama ilivyo kwenye Mikoa mingine ambayo inafanya vizuri kwenye sekta hii muhimu kwa uchumi wa Nchi, lakini kipato cha Mtanzania mmoja mmoja," aliongeza.

Kwa upande wake, Kamishma Msaidizi Mwandamizi wa TFS Kanda ya kati, Bwn. Mathew Kiondo, amesema Wakala unatekeleza mikakati mbalimbali kwa ajili ya kuboresha vivutio vya Utalii vilivyopo kanda ya kati.

"Baadhi ya vituo vya Utalii vilivyopo Dodoma, ikiwemo Mlima wa Hanang na Kituo cha michoro ya kale ya miambani cha Kondoa Irangi vinahusisha mapori ya nisitu ya akiba, misitu ambayo sisi TFS tunafanya kazi kubwa ya kuiendeleza na kuilinda Ili kuchochea Utalii wa mazingira," alieleza.

Naye Bwn. George Mwagane, Afisa Utalii Mwandamizi , Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Kanda ya Kati, amesema Bodi inatekeleza programu maalumu ya kivitangaza vituo vya  Utalii vya Kanda ya kati, Kitaifa na kimataifa.

Amesema, jitihada kubwa zilizofanywa na Serikali kuufungua Mkoa wa Dodoma kiuchumi, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Reli ya Treni ya Umeme ya mwendokasi (SGR), pamoja na mradi unaokaribia kukamilika wa ujenzi wa  uwanja wa ndege wa kimataifa wa Msalato zinatoa fursa na mchango mkubwa katika kuchochea shughuli za sekta ya Utalii Mkoani Dodoma.



Bwn. Zuberi Mabie


Kwa upande wake, Bwn. Zuberi Mabie, Meneja wa Kituo cha michoro ya kale cha Kondoa Irangi, alisema eneo hilo limeendelea kuvutia idadi kubwa ya watalii kutoka ndani na nje ya Nchi.

Amebainisha sababu zinazochangia mabadiliko hayo chanya kuwa ni pamoja na uwekezaji mkubwa ambao Serikali imeufanya katika eneo hilo, ikiwa ni pamoja na uboreshaji wa miundombinu ya barabara, huduma bora za kitalii na kijamii, pamoja na kukitangaza kitvutio hicho Kitaifa na kimataifa.


"Katika kipindi cha mwaka 2018 Kituo kilipokea jumla ya watalii 1, 287 Kutoka ndani ya nchi, ambapo mwaka 2020 idadi ya watalii wa ndani ilikuwa 2,142 na mwaka 2021 watalii 3,335," alieleza.

Mwaka 2022, Bwn. Mabie alisema jumla ya watalii wa ndani ya nchi waliotembelea kituo hicho walikuwa 4,763, idadi ambapo iliongezeka na kufikia watalii 6,229 mwaka 2023, na mwaka 2024 jumla ya watanzania 7,654 walivutiwa na Kituo hicho cha kihistoria.


Kwa upande wa watalii wa kimataifa, mwaka 2018 walikuwa 664, ambapo mwaka 2020 idadi ilikuwa watalii 171, na mwaka 2021 tulipokea jumla ya watalii  243 Kutoka nje ya Nchi," aliongeza.


Akieleza zaidi juu ya mwendo mzuri wa watalii wanaotembelea kivutio hicho cha michoro ya kale, alisema mwaka 2022, jumla ya watalii wa kimataifa 428 walitembelea kituo, ambapo mwaka 2023 idadi ilipanda na kufikia watalii 671.

"Na katika kipindi cha mwaka 2024, tulitembelewa na jumla ya watalii 541 kutoka nje ya Tanzania," alisema.

Katika kuazimisha siku ya Utalii Duniani ,ambayo kwa mwaka huu iliazimishwa Tarehe 27, Septemba  kwa kauli mbiu ya "Utalii Na Maendeleo Endelevu" zaidi ya wakazi 40 kutoka Jiji la Dodoma, wakiwemo watumishi Kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, TFS, TTB na kwenye Taasisi mbalimbali za Umma na sekta binafsi walifanya ziara ya siku mbili katika kituo cha michoro ya kale ya kwenye miamba ya Kolo, Wilayani Kondoa.

Post a Comment

Previous Post Next Post