"Wanawake Kutoshirikishwa Katika Umiliki Na Urithi Wa Ardhi, Taratibu Za Kimila Na Mitazamo Ya Kijamii Yenye Mfumo Dume Nara Nyingi Huwazuia Wanawake Kupata Umiliki Wa Ardhi Ulio Salama,"
Na Mwandishi wetu
DODOMA. WANAWAKE wanaoishi maeneo ya vijijini wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa rasilimali muhimu, hali ambayo huchangiwa na kuwepo kwa mfumo dume.
Hayo yamesemwa na Mratibu wa Taifa wa Private Security Gender and Human Rights Platform (PRISEP), Bi. Yvonne Mtango wakazi wa mkutano wa kuwasilisha ripoti yenye lengo la kukuza sauti za wanawake wa ngazi ya jamii katika usimamizi wa ardhi na mabadiliko ya tabianchi.
Mashirika shiriki katika mkutano huo yalikuwa ni pamoja na Shirika lisilo la kiserikali la Women Action Towards Economic Development) in Tanzania, (WATED,Women Action on Eco-health And Legal Rights (WAE-HEAL), na Tree of Hope.
Bi. Mtango alisema kuwa wanawame wamekuwa wakikabiliwa na vikwazo vya kimuundo katika ushiriki wa maamuzi na upatikanaji wa rasilimali.
Alisema kuwa Sera ya Taifa ya Ardhi (2023) Imeboreshwa kutoka NLP ya mwaka 1995 ili kupunguza migogoro ya ardhi, ili kutambua haki za wanawake kumiliki, kurithi na kuhamisha ardhi.
Alisema kuwa lengo ni kuendeleza usawa wa kijinsia, usalama wa chakula na usimamizi endelevu wa ardhi.
"Sera hii inaunga mkono hatua za kitaifa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.Sera hii ni fursa muhimu ya kushughulikia changamoto za kimsingi za haki za ardhi kwa wanawake," alisema
Akizungumzia wanawake walio pembezoni na raslimali, alisema kuwa wanakabiliwa na ukosefu wa usalama katika upatikanaji wa ardhi na rasilimali, na kwamba uhai wao wa kiuchumi hukwamishwa na vikwazo vya kimfumo wa kijamii kama kilimo.
"Udhaifu huu unaonekana zaidi kwa wanawake walioko pembezoni, ambapo upatikanaji wao wa rasilimali muhimu hukumbwa na changamoto za mfumo dume mara kwa mara.," alisema
Aidha akizungumzia mabadiliko ya tabianchi na jinsia alisema kuwa ukame, mafuriko na mvua zisizotabirika zimekuwa zikiathiri zaidi uchumi wa wanawake.
Aliongeza kuwa, kundi linaloathirika zaidi ni wanawake wanaotegemea rasilimali asili (mvua) ambayo uathiri pia na kipato (kilimo).
" Wanawake na majukumu yao ya kifamilia, hubeba mzigo mkubwa wa changamoto za tabianchi," aliongeza.
Alisema kuwa mradi unalenga kuimarisha sauti za wanawake ili kusimamia utekelezwaji wa sera shirikishi za mabadiliko ya tabianchi
Pia alisema changamoto za mila na mfumo dume mara nyingi hupuuza haki za kisheria kwa wanawake.
" Wanawake kutoshirikishwa katika umiliki na urithi wa ardhi, taratibu za kimila na mitazamo ya kijamii yenye mfumo dume mara nyingi huwazuia wanawake kupata umiliki wa ardhi ulio salama,"alisema
Akizungumzia mwanya kati ya sera za ardhi na utekelezwaji wake katika ngazi ya jamii, alisema wanawake vijijini bado wanakabiliwa na changamoto za umiliki salama wa ardh, huku mila na mfumo dume zikionekana kudhoofisha haki za wanawake katika umiliki wa ardhi.
"Wanawake wanapata nafasi ndogo katika mchakato wa kufanya maamuzi, hivyo, kunauhitaji wa mbinu jumuishi na zinazoheshimu tamaduni katika utawala wa ardhi na tabianchi"alisema
Naye,Mratibu wa Shirika lisilo la kiserikali la Women Action Towards Economic Development) in Tanzania (WATED, Bi. Maria Matui alisema kuwa mikutano huo ulikuwa kwa ajili ya kupitisha taarifa baada ya kupokea maoni mbalimbali katika mikoa ya Ruvuma, Morogoro, Iringa, Mwanza, Kagera, Geita, Arusha na Tanga.
Alisema kuwa mbinu zilizotumika ni pamoja na midahalo ya ngazi ya jamii, mafunzo, mapitio ya sera za ardhi na tabianchi, mahojiano na wadau muhimu kutoka mashirika ya kiraia (CSOs).
Kwa upande wake,mshiriki kutoka Ifakara, Morogoro, Bi.Ebenita Chamanga alisema Serikali pamoja na mashirika yasiyo ya kiserikali yamekuwa yakiweka jitihada ili wananchi waweze kupata elimu juu ya umiliki wa ardhi, mabadiliko ya tabia nchi na hata kwenye suala la ukatili wa kijinsia.
Chamanga ambaye anatoka kwenye Asasi ya Wanawake na Watoto alisema kuwa wamekuwa wakielimisha wanawake umuhimu wa kuingia kwenye kamati za vijiji ambapo masuala mbalimbali ikiwemo ardhi, mabadiliko ya tabia nchi na hata malezi ya watoto huwa yanaongelewa.
Post a Comment