NFRA KUTUMIA SH BILIONI 6.2 KUJENGA MAKAO YAKE MAKUU JIJINI DODOMA




                     MUKTASARI

👉   Ujenzi wa Makao hayo Makuu ya NFRA utahusisha ujenzi wa ofisi za watumishi, maabara ya kisasa ya uchunguzi wa nafaka pamoja na kituo maalumu cha kutoa huduma za zana za kisasa za kilimo


DODOMA. WAKALA wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula  (NFRA) umetenga kiasi cha Shilingi Bilioni 6.2 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa makao makuu ya ofisi za wakala Jijini  Dodoma.

Mradi huo mkubwa unaotarajia kutekelezwa kwenye kipindi cha mwaka huu wa fedha wa 2025/26, utahusisha ujenzi wa ofisi za watumishi, maabara ya kisasa ya uchunguzi wa nafaka pamoja na kituo maalumu cha kutoa huduma za zana za kisasa za kilimo.

Katika mahojiano maalumu na 'Swahili News'  Mkurugenzi Mtendaji wa NFRA, Dkt. Andrew Komba amesema mradi huo utatekekezwa katika eneo la Mahomanyika, pembezoni mwa Jiji la Dodoma.


Mkurugenzi Mtendaji wa NFRA, Dkt Andrew Komba 


"Tumepata eneo kubwa katika eneo la Mahomanyika ambapo tunatarajia kuanza ujenzi wa ofisi zetu za makao makuu," alisema.

 

Amesema fedha za ujenzi wa mradi huo zinatoka kwenye bajeti kuu ambayo NFRA imepanga kuitumia katika mwaka huu wa fedha, ya Shilingi Trilioni 1.2.

Katika kuboresha ufanisi wa shughuli zake, Dkt Komba amesema katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2024/25, NFRA ilifanya maboresha makubwa katika muundo wake, hatua ambayo ililenga kuiwezesha Wakala kuendesha shughuli zake kwa mlengo wa kibiashara zaidi.

"Kupitia mfumo huu mpya, tutaendelea na jukumu letu la msingi la kuhakikisha usalama wa chakula nchini kwa njia ya kununua na kukusanya nafaka nyingi ghalani," alisema.

Aliongeza, kwa upande wa mlengo wa biashara, NFRA itatumia ziada ya nafaka kwa ajili ya kuuza kwenye Nchi za jirani zenye uhitaji.

"Mpaka sasa, tunauza nafaka kwenye Nchi za Kenya, Malawi na Zambia, na tunatarajia kufungua masoko mapya katika Nchi za Zimbabwe na DRC Congo," aliongeza.

Katika mwaka huu wa fedha, NFRA imepanga kutumia Shilingi Trilioni 1.2 kwa ajili ya kuendesha  shughuli zake, pamoja na kutekeleza miradi ya kimkakati inayolenha kuongeza uwezo wake wa kuhifadhi nafaka.

Miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa maghala mapya ya kuhifadhia nafaka, uanzishaji wa vituo maalumu vya kutoa huduma ya mitambo (zana) za kilimo kwa wakulima pamoja na ununuzi wa nafaka.

Miradi inatarajia kuongeza kiwango cha uhifadhi wa nafaka kutoka tani 776,00 kwa sasa hadi kufikia  tani milioni 1.1 ndani ya mwaka huu wa fedha.

Katika msimu wa mwaka huu wa ununuzi wa mazao unaotarajia kuzinduliwa wiki hii, NFRA inatarajia kutumika Shilingi Bilioni 860.

"Tunatarajia kununua takribani tani 800,000 za mahindi, tani 150,000 za mpunga, mazao mengine tutakayonunua na kuhifadhi ni pamoja na mazao ya jamii ya kunde, alizeti na sukari,"Dkt Komba ameeleza.


Post a Comment

Previous Post Next Post