TFS YAWANOA WATAALAMU MFUMO WA MBEGU, KUIMARISHA USIMAMIZI WA MBEGU NCHINI


👉 Kuanzishwa kwa mfumo wa SEEDMIS kunalenga kuondoa changamoto ya kukosekana kwa takwimu sahihi za mbegu na miche ya miti.


Na Mwandishi Wetu

MOROGORO: Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) umeendesha kikao kazi cha mafunzo kuhusu mfumo wa uzalishaji na usimamizi wa mbegu (SEEDMIS) katika Kituo cha Mbegu Morogoro, ikiwa ni hatua muhimu ya kuimarisha upatikanaji wa mbegu bora na takwimu sahihi katika sekta ya misitu nchini.

Mafunzo hayo yaliyofanyika Aprili 24 na 25, 2026, yamewakutanisha makamanda wa kanda, wahifadhi wa mashamba ya miti, wasimamizi wa vituo vya mbegu pamoja na wakuu wa vitengo mbalimbali wa TFS, kwa lengo la kuwajengea uelewa wa pamoja juu ya mbinu bora za uzalishaji, ukusanyaji na utunzaji wa mbegu.

Akizungumza katika kikao hicho, Kamishna Msaidizi Muandamizi na Meneja wa Biolojia ya Mbegu za Miti, Fandey Mashimba, alisema kuanzishwa kwa mfumo wa SEEDMIS kunalenga kuondoa changamoto ya kukosekana kwa takwimu sahihi za mbegu na miche ya miti.


Alisema kwa muda mrefu matumizi ya mifumo ya karatasi yamekuwa yakisababisha upotevu wa taarifa muhimu katika mnyororo mzima wa uzalishaji wa mbegu, hali iliyokuwa ikiathiri upangaji na ufuatiliaji wa rasilimali hizo.

“Mfumo wa SEEDMIS utasaidia kurahisisha ukusanyaji, uhifadhi na uchambuzi wa takwimu za mbegu na miche ya miti kwa wakati halisi, hivyo kuongeza ufanisi katika maamuzi ya kitaalamu,” alisema Mashimba.

Kwa upande wake, Naibu Kamishna wa Uhifadhi anayeshughulikia Masoko na Matumizi Endelevu ya Rasilimali za Misitu, Salehe Beleko, aliyemwakilisha Kamishna wa Uhifadhi wa TFS, alielekeza kuwa kuanzia sasa usambazaji wa miche pamoja na taarifa au takwimu zake lazima zipitie mfumo wa SEEDMIS ili kutambuliwa rasmi.

Alisisitiza kuwa takwimu zozote ambazo hazitatokana na mfumo huo hazitahesabika kama takwimu rasmi za taasisi, akiwataka Wakuu wa Kanda (ZCC) na Wahifadhi Wakuu wa Mashamba kuhakikisha wanasimamia kikamilifu utekelezaji wa maelekezo hayo kwa watumishi walio chini yao.

Naye Naibu Kamishna wa Uhifadhi anayeshughulikia Kurugenzi ya Mbegu, Dkt. Hamza Katety, alisema bado kuna changamoto ya usahihi wa takwimu katika mnyororo wa uzalishaji wa mbegu na miche, hali inayohitaji maboresho ya haraka.

Alisema kuongezwa kwa moduli mbalimbali ndani ya mfumo wa SEEDMIS ni takwa la kitaasisi lililopitishwa na uongozi wa juu wa TFS, na kwamba utekelezaji wake unapaswa kufanyika katika bustani zote za miche nchini ili kuhakikisha takwimu zinakuwa sahihi na zenye kuaminika.


Aidha, alisisitiza kuwa mafunzo hayo ni muhimu katika kuhakikisha wataalamu wa TFS wanakuwa na uelewa wa pamoja kuhusu matumizi ya mfumo huo, hatua itakayosaidia kuongeza tija na ubora wa miche ya miti inayozalishwa nchini.

Washiriki wa kikao hicho walieleza kuwa matumizi ya mifumo ya kidijitali kama SEEDMIS yataongeza uwazi na ufanisi katika usimamizi wa rasilimali za misitu, sambamba na kuimarisha juhudi za uhifadhi wa mazingira.

TFS imeendelea kusisitiza matumizi ya teknolojia katika kuboresha huduma zake, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa miche bora kwa ajili ya kampeni mbalimbali za upandaji miti nchini.







Post a Comment

Previous Post Next Post