KAMPUNI YATANGAZA MAPINDUZI YA BIASHARA YA MAZAO YA MISITU


MUHTASARI 

Wananchi wanaotembelea banda la TFS wanapata fursa ya kujifunza kuhusu mnyororo wa thamani wa mazao ya misitu na nyuki, ikiwemo asali, nta na bidhaa nyingine zinazozalishwa kwa kuzingatia viwango vya ubora.

DAR ES SALAAM: Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya Misitu, kampuni tanzu ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Bwn. Fortunatus Mhambe amesema kampuni hiyo imejipanga kuwa miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa bidhaa za misitu na nyuki zenye ubora wa kimataifa, huku ikilenga kupanua masoko ya ndani na nje ya nchi ili kuongeza mchango wa sekta ya misitu katika ukuaji wa uchumi wa Taifa.

Mhambe ametoa kauli hiyo alipotembelea banda la Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia TFS katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), ambapo aliwataka wananchi, wafanyabiashara na wawekezaji kutumia maonesho hayo kujionea bidhaa mbalimbali zinazozalishwa na Kampuni ya Misitu pamoja na kupata elimu kuhusu fursa zilizopo katika sekta ya misitu na nyuki.

“Tunawakaribisha Watanzania wote kufika katika banda la TFS kujionea bidhaa zetu zinazotokana na misitu na nyuki pamoja na kujifunza kuhusu fursa mbalimbali zilizopo. Dhamira yetu ni kuijenga Kampuni ya Misitu kuwa miongoni mwa kampuni kubwa nchini zinazozalisha na kuuza bidhaa za misitu katika masoko ya ndani na kimataifa,” amesema Mhambe.

Amesema maonesho ya Sabasaba ni jukwaa muhimu la kuitangaza Kampuni ya Misitu na kuonesha uwezo wake katika kuongeza thamani ya mazao ya misitu na nyuki kupitia uzalishaji wa bidhaa zinazokidhi viwango vya ubora vinavyohitajika katika soko la ndani na nje ya nchi.

Kwa mujibu wa Mhambe, wananchi watakaotembelea banda la TFS watapata fursa ya kujifunza kuhusu mnyororo wa thamani wa mazao ya misitu na nyuki, ikiwemo asali, nta na bidhaa nyingine zinazozalishwa kwa kuzingatia viwango vya ubora, sambamba na kupata taarifa za uwekezaji na biashara zinazopatikana kupitia sekta hiyo.

Amesema mkakati wa Kampuni ya Misitu wa kuongeza thamani ya rasilimali za misitu kwa njia endelevu unalenga kuchochea ajira, kuongeza kipato cha wananchi, kupanua wigo wa biashara na kuimarisha mchango wa sekta ya misitu katika maendeleo ya uchumi wa Taifa.

Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania unaendelea kuwakaribisha wananchi kutembelea banda lake katika Maonesho ya 50 ya Sabasaba ili kujionea bidhaa mbalimbali za misitu na nyuki, kupata elimu kuhusu uhifadhi wa misitu na kufahamu fursa za uwekezaji na biashara zinazotokana na rasilimali za misitu.




Post a Comment

Previous Post Next Post