MATUMIZI YA MIFUMO YA KIDIGITALI KIPAUMBELE KWA VYAMA VYA USHIRIKA NCHINI

MUHTASARI 

Matumizi ya mifumo ya kidigitali yataongeza uwazi, ufanisi na usalama katika shughuli za vyama vya ushirika, huku yakisaidia kupunguza changamoto za udanganyifu ambazo zimekuwa zikijitokeza katika baadhi ya maeneo.

MRAJIS Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Mwanza, Bi. Hilda Boniphace, amesema Tume ya Maendeleo ya Ushirika imeendelea kuhimiza matumizi ya mifumo ya kidigitali kwa vyama vya ushirika nchini, ikiwa ni moja ya vipaumbele nane vilivyowekwa kwa lengo la kuwawezesha wanaushirika kunufaika na teknolojia za kisasa zisizo na uwezekano wa kufanyiwa udanganyifu.

Ameyasema hayo Mei 28, 2026, wakati wa ufunguzi wa Jukwaa la Maendeleo ya Ushirika Mkoa wa Mwanza linalofanyika kwa muda wa siku mbili hadi Mei 29.


Akizungumza katika jukwaa hilo, Bi. Hilda amesema matumizi ya mifumo ya kidigitali yataongeza uwazi, ufanisi na usalama katika shughuli za vyama vya ushirika, huku yakisaidia kupunguza changamoto za udanganyifu ambazo zimekuwa zikijitokeza katika baadhi ya maeneo.

Katika kuhakikisha kipaumbele hicho kinafikiwa, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Climb Up Limited, Bwn. Emmanuel Ngallah, katika wasilisho lake kwenye jukwaa hilo amesema wamefika Jijini Mwanza kuleta suluhisho na tabasamu kwa wanaushirika pamoja na wananchi kwa ujumla kupitia mifumo madhubuti ya kidigitali inayolenga kuondoa changamoto za udanganyifu.

Amesema kampuni hiyo imejikita katika utoaji wa teknolojia za kisasa ikiwemo mifumo ya kidigitali na mizani janja ambayo itasaidia kuongeza uaminifu na usahihi katika shughuli za biashara na ushirika.

Kwa upande wao, baadhi ya washiriki wa jukwaa hilo walieleza kufurahishwa na elimu waliyoipata kuhusu matumizi ya mifumo ya kidigitali na mizani janja, wakisema imewapa uelewa mkubwa kuhusu namna teknolojia inavyoweza kuboresha shughuli zao za kila siku.

Jukwaa hilo la Maendeleo ya Ushirika Mkoa wa Mwanza linatarajiwa kuendelea hadi Mei 29, likiwa limewakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya ushirika kujadili namna bora ya kutumia teknolojia za kisasa kuimarisha uwazi, kuongeza ufanisi na kuleta maendeleo kwa wanaushirika nchini.




Post a Comment

Previous Post Next Post