👉 TFS pamoja na taasisi zisizo za kiserikali zimetakiwa kuongeza juhudi katika utoaji wa elimu ya mazingira kwa jamii, ili kupunguza vitendo vya ukataji na uchomaji wa misitu hovyo vinavyochangia uharibifu wa mazingira.
Na Valentine Oforo
WAKALA wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwa kushirikiana na Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Mhe. Dustan Kyobya, wameadhimisha Miaka 62 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa kupanda jumla ya miti 2,000 katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha uhifadhi wa mazingira.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo lililofanyika katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Ifakara, Kyobya amesema upandaji miti ni hatua muhimu katika kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi na kulinda vyanzo vya maji, huku akiwahimiza wananchi kushiriki kikamilifu katika kulinda mazingira yao.
Amesema ni wajibu wa kila mwananchi kuhakikisha anapanda na kutunza miti ili kuendeleza rasilimali za misitu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho, akisisitiza umuhimu wa kudumisha amani, umoja na mshikamano kama msingi wa maendeleo endelevu.
Mhe. Kyobya pia ameitaka TFS pamoja na taasisi zisizo za kiserikali kuongeza juhudi katika utoaji wa elimu ya mazingira kwa jamii, ili kupunguza vitendo vya ukataji na uchomaji wa misitu hovyo vinavyochangia uharibifu wa mazingira.
Kwa upande wake, Mhifadhi wa Misitu TFS Wilaya ya Kilombero, Zarina Haridi, amesema zoezi hilo limefanikiwa kupanda miti 500 katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Ifakara na miti 1,500 katika Halmashauri ya Mlimba, hatua inayolenga kurejesha uoto wa asili katika maeneo yaliyoharibika.
Amesema TFS itaendelea kushirikiana na wananchi na wadau mbalimbali kuhakikisha juhudi za uhifadhi zinakuwa endelevu na zenye matokeo chanya kwa jamii.
“Tunawahamasisha wananchi kujitokeza kuchukua miche ya miti bure kutoka TFS na kupanda katika maeneo yao ili kurejesha uoto wa asili na kulinda mazingira,” amesema Zarina.
Ameongeza kuwa mafanikio ya juhudi hizo yanategemea ushiriki wa pamoja kati ya serikali, taasisi na wananchi, huku akisisitiza kuwa utunzaji wa mazingira ni jukumu la kila mmoja.
Maadhimisho ya Siku ya Muungano yameendelea kuwa jukwaa muhimu la kuhamasisha shughuli za maendeleo na uhifadhi wa mazingira, huku TFS ikiendelea kuonyesha mfano kwa vitendo kupitia kampeni za upandaji miti nchini.







Post a Comment