SERIKALI YAWAPIGA MSASA WANAFUNZI, WALIMU CHUO CHA MIPANGO JUU YA DIRA 2050

 


Muhtasari

👉 Serikali inatekeleza afua mbalimbali za kuimarisha sekta ya uendelezaji wa rasilimali watu nchini kwa kuboresha utendaji wa Taasisi za elimu ya juu ili kuzalisha wataalamu wenye ujuzi unaoendana na maono ya kiuchumi Tanzania.

Na Valentine Oforo, Dodoma 

DODOMA: OFISI ya Rais, (Mipango na Uwekezaji) imeendesha warsha mtaalamu ya kuwajengea uwezo Wanafunzi na Walimu wa Chuo Cha Mipango Jijini Dodoma (IRDP) juu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Warsha hiyo iliyofanyika kwa muda wa saa mbili iliongozwa na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mipango na Uwekezaji) Dkt. Pius Stephen Chaya.

Akiwasilisha mada husika, "Kupanga Mustakabali wa Tanzania: Jukumu la Uendelezaji Maeneo ya Vijijini katika Kufikia Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2050," Dkt. Chaya alisisitiza kuwa vijana wana mchango mkubwa katika kutimiza maono ya Dira 2050.


"Chuo hiki ni miongoni mwa Taasisi muhimu katika kusaidia Taifa la Tanzania kufikia malengo  ya Dira ya Maendeleo ya mwaka 2050," alisema.

Alieleza kwamba utekelezaji wa mpango huu wa muda mrefu wa kiuchumi utahusisha uwekezaji mkubwa katika maeneo ya vijijini, maeneo ambayo yana ardhi kubwa, na ndiyo makazi ya idadi kubwa ya wananchi.


"Mafunzo yanayotolewa na Chuo Cha Mipango yanajikita katika nyanja mbalimbali za uendelezaji maendeleo vijijini, hii inamaanisha kuwa mna jukumu kubwa katika kuisaidia Serikali kufikia maono ya Dira ya Taifa ya maendeleo" aliongeza.

Dkt. Chaya alifafanua zaidi kwamba Serikali inatekeleza afua mbalimbali za kuimarisha sekta ya uendelezaji wa rasilimali watu nchini kwa kuboresha utendaji wa Taasisi za elimu ya juu ili kuzalisha wataalamu wenye ujuzi unaoendana na maono ya kiuchumi Tanzania.

"Dira hii inalenga kuinua pato la Taifa (GDP) kufikia Dola za Marekani trilioni moja kwa mwaka, huku kipato kwa kila mtu kikifikia wastani wa dola 7,000," alibainisha.

Ili kufikia malengo hayo, alisisitiza umuhimu wa kuhusisha vijana na sekta binafsi, ambayo inatarajiwa kuchangia angalau asilimia 70 ya pato la Taifa.


"Hakikisheni mnapata nakala ya Dira 2050, msome kwa makini, na kubaini sehemu ambazo mnaweza kuchangia katika utekelezaji wake," alishauri.

Dkt.  Chaya aliupongeza uongozi wa Chuo Cha IRDP kwa kuandaa warsha hilo na kutoa wito kwa Taasisi zingine za elimu nchini kuiga mfano huo mzuri na wa kizalendo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha IRDP, Prof. Hozen Mayaya alieleza kufurahishwa na ufanisi wa warsha hiyo.

Alisema chuo kimeandaa warsha hiyo ili kuwapa fursa wanafunzi kuelewa kwa kina juu ya Dira ya Maendeleo 2050 ambayo itaanza kutekelezwa rasmi mwezi Julai mwaka huu.

"Tunashukuru sana kwa namna ambayo Dkt. Chaya amekubali kuja na kutujengea uwezo kuhusu utekelezaji wa Dira 2050," Prof. Mayaya alisema.

Aliahidi kwamba Chuo hicho cha umma kitaendelea kuandaa programu mbalimbali zinazolenga kuwajengea uwezo wanafunzi kushiriki kikamilifu  katika shughuli za kujenga  uchumi wa Taifa.


Prof. Mayaya pia aliipongeza serikali kwa kuendelea kutoka misaada mbalimbali ya kuboresha miundombinu na vifaa vya mafunzo katika chuo hicho kilichopo pembezoni mwa Jiji la Dodoma.




Post a Comment

Previous Post Next Post