DODOMA. KATOTO Sports Academy (KSA), Taasisi inayoongoza nchini Tanzania kwa kuibua, kukuza na kuendeleza vipaji vya mchezo wa Tennis kwa watoto, imezindua viwanja vipya vya kisasa vya mchezo huo Jijini Dodoma.
Sherehe za uzinduzi wa viwanja hivyo imefanyika kwa siku mbili, Tarehe 29 na 30 mwezi Novemba 2025, katika eneo la uwekezaji la Njedengwa, nje kidogo ya Jiji la Dodoma.
Uwekezaji huo mkubwa wa viwanja hivyo unaakisi jitihada za Taasisi ya Katoto Tennis kukuza ufanisi wa mchezo wa Tennis nchini Tanzania, kwa jicho la kuandaa wachezaji hodari watakao iwakilisha nchi ya Tanzania katika mashindano mbalimbali ya kikanda, kimataifa, pamoja na kuchochea kasi ya kufanyika kwa mashindano ndani ya nchi.
Sherehe za uzinduzi wa viwanja zilikwenda sambamba na mashindano maalumu kwa watoto, na baadae watu wazima, ambapo zaidi ya wachezaji watoto hamsini Kutoka mikoa mbalimbali walishindana.
Mikoa husika ni pamoja na Dar es Salaam, Arusha, Morogoro na wenyeji Dodoma.
Akitoa hotuba kwenye tukio hilo la kihistoria, na la kwanza kufanyika Jijini Dodoma, Mgeni Rasmi, Bwn. Nadim Aziz Yusufu aliipongeza Taasisi ya Katoto Sports Academy kwa kuwekeza katika tasnia ya mchezo wa Tennis nchini Tanzania.
"Wadau wengi wa michezo nchini Tanzania wamekuwa wakielekeza pesa nyingi katika kudhamini mchezo wa mpira wa miguu, na michezo mingine michache, ila siyo Tennis," alisema.
Kutokana na hatua hiyo, amesema mpaka sasa Tanzania ina viwanja vichache sana vya Tennis, hali ambayo inadhoofisha jitihada za kukuza mchezo huo.
"Leo hii, viwanja vya Tennis vichache sana vipo Dar es Salaam, Arusha na Morogoro, hivyo uwekezaji huu mkubwa hapa Jijini Dodoma utatoa msukumo mkubwa katika kuendeleza mchezo huu wa Tennis nchini Tanzania," aliongeza.
Aidha, Bwn. Yusufu amewataka wadau wengine kuiga mfano mzuri ulioonyeshwa na KSA katika kukuza vipaji na ufanisi wa tasnia hiyo ya michezo nchini.
Kwa upande wake, Mratibu Mkuu wa shughuli za Taasisi, Bwn. Pauli Ingavi amesema uwekezaji huo pia unahusisha ujenzi wa miundombinu ya kisasa ya michezo mingine, nje ya Tennis.
"Kwa sasa ujenzi wa kituo unaendelea, ambapo hadi kukamilika kwake kituo hiki kitakuwa na miundombinu ya kisasa ya kufundishia na kufanyia mashindano ya michezo ya mpira wa pete, mpira wa mikono, taikondo, mpira wa miguu, mpira wa meza, na michezo mingine mingi," alisema Bwn. Ingavi ambaye pia ni Kocha Mkuu wa Taasisi.
Pamoja na hayo, Bwn. Ingavi amesema ujenzi wa kituo unahusisha ufungaji wa huduma za bure za intaneti, migahawa ya kisasa ya kuuzia kahawa, juisi, vyakula na bidhaa nyingine muhimu.
"Maono yetu ni kulifanya eneo hili kuwa sehemu nzuri ya kutoa huduma ya Utalii wa michezo, na tunatatajia kuwekeza kikamilifu kwenye miradi ya ufugaji ea Kuku wa kienyeji, Kanga, Bata, Sungura, Samaki na mfugo mingine rafiki kwa mazingira," aliongeza.
Alisema kituo kitakuwa kikitoa huduma za chakula kwa kupitia kauli mbiu ya "Kutoka Shambani Hadi Mezani" , ambapo wateja watapatiwa fursa ya kwenda kwenye eneo la mifugo na kukamata mfugo anaotaka Ili aandaliwe, hatua ambayo itatoa fursa ya wateja kushiriki katika mazoezi.
"Baada ya kukamilisha ujenzi wa kituo, eneo hili litakuwa huru kwa wadau, Taasisi na watu binafsi kukodisha kwa ajili ya kufanyia shughuli mbalimbali, ikiwa ni pamoja na mashindano ya michezo mbalimbali, mabonanza, harusi na shughuli nyingine za kijamii," Bwn. Ingavi aliweka wazi.
Katika mashindano ya uzinduzi wa viwanja hivyo, washindi katika shindano la watoto walipatiwa makombe mbalimbali huku kwa upande wa shindano la wakubwa washindi waliondoka na zawadi za pesa taslimu.

.jpg)

Post a Comment