MUHTASARI
Serikali yawahimiza wananchi kuendelea kuunga mkono juhudi za kuongeza uoto wa asili kupitia kampeni mbalimbali za upandaji miti zinazolenga kuifanya Tanzania kuwa ya kijani zaidi ifikapo mwaka 2050.
Na Mwandishi Wetu, Kilombero
WAKALA wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Wilaya ya Kilombero umeadhimisha Siku ya Mazingira Duniani kwa kupanda miti 1,000 katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo, huku wananchi wakihimizwa kuacha shughuli zinazoharibu mazingira na kushiriki kikamilifu katika uhifadhi wa rasilimali za asili.
Shughuli hiyo ilifanyika chini ya kampeni ya kitaifa ya “Dira ya 2050: Tunakijanisha Tanzania” na kuongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Mhe. Wakili Dunstan Kyobya, aliyekuwa mgeni rasmi.
Alisema vitendo vya uharibifu wa mazingira vinaendelea kuchangia kupungua kwa vyanzo vya maji, kuongezeka kwa athari za mabadiliko ya tabianchi na kuhatarisha shughuli muhimu za kiuchumi, hususan kilimo na ufugaji.
"Ni wajibu wa kila mmoja wetu kushiriki katika kulinda mazingira kwa kupanda miti, kutunza vyanzo vya maji na kuacha shughuli zinazochangia uharibifu wa mazingira. Haya ni maeneo muhimu kwa maisha ya sasa na ya baadaye,” alisema.
Mhe. Kyobya aliwataka wananchi kuepuka shughuli za kibinadamu katika maeneo yaliyohifadhiwa na kandokando ya mito, akieleza kuwa maeneo hayo yana mchango mkubwa katika kulinda mifumo ikolojia na kuhakikisha upatikanaji endelevu wa maji.
Aidha, aliwahimiza wananchi kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali za kuongeza uoto wa asili kupitia kampeni mbalimbali za upandaji miti zinazolenga kuifanya Tanzania kuwa ya kijani zaidi ifikapo mwaka 2050.
Kwa mujibu wa Mhifadhi waTFS Wilaya ya Kilombero, SCO Zarina Haridi, miti 1,000 iliyopandwa ni sehemu ya mchango wa wilaya hiyo katika utekelezaji wa kampeni ya kitaifa ya kuimarisha uhifadhi wa mazingira na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Maadhimisho ya mwaka huu nchini yamefanyika chini ya kaulimbiu ya “Dira ya 2050: Tunakijanisha Tanzania,” inayolenga kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika urejeshaji wa mifumo ikolojia, utunzaji wa mazingira na kuongeza uoto wa asili nchini.






