MUHTASARI
Lengo kuu la ujenzi wa bandari hiyo ni kuimarisha mnyororo wa thamani wa mazao ya uvuvi kwa kuwezesha uhifadhi bora, uchakataji wa kisasa na upatikanaji wa masoko yenye tija zaidi.
MKUU wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Zainab Telack, amesema Bandari ya Uvuvi ya Kilwa Masoko, ambayo iliahidiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ipo tayari kuanza kutoa huduma baada ya kufikia hatua za mwisho za ukamilishaji wake.
Akizungumza wilayani Kilwa mkoani Lindi wakati wa zoezi la kihistoria la majaribio ya mitambo na miundombinu mbalimbali ya bandari hiyo, Mhe. Telack amesema kiwango cha ukamilishaji wa mradi huo kimefikia asilimia 99.99, huku hatua iliyobaki ikiwa ni kuwasha na kuthibitisha utendaji wa mitambo mbalimbali.
Amesema miongoni mwa majaribio yaliyofanyika leo ni pamoja na kuwasha mitambo ya kuzalisha barafu, ambayo inauwezo wa kuzalisha barafu tani 100 kwa siku mitambo hiyo inauwezo wa kugandisha barafu kwa nyuzi joto 3 sentigredi.
“Hii ni ishara kuwa Bandari yetu sasa iko tayari kuanza kazi, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ameandika historia kwa kujenga Bandari ya kwanza ya kisasa ya uvuvi nchini, ambayo itafungua fursa nyingi za kiuchumi kwa wananchi na wadau wa sekta ya uvuvi,”amesema Mhe. Telack.
Mhe. Telack amesema ameridhishwa na ubora wa kazi iliyofanyika pamoja naa ufanisi wa mitambo iliyowekwa, huku akimpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maono yake ya kuidhinisha zaidi ya shilingi bilioni 280 kwa ajili ya ujenzi wa mradi huo mkubwa wa kimkakati.
Aidha, ameipongeza Wizara ya Mifugo na Uvuvi chini ya uongozi wa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, kwa usimamizi madhubuti wa utekelezaji wa mradi huo hadi kufikia hatua ya mwisho ya ukamilishaji wake.
Mhe. Telack pia amewahimiza wavuvi na wadau wote wa sekta ya uvuvi kuanza kujipanga kutumia fursa zitakazotokana na uwepo wa bandari hiyo ya kisasa, akieleza kuwa mradi huo utarahisisha shughuli za uvuvi, uhifadhi na biashara ya mazao ya uvuvi katika soko la ndani na nje ya nchi.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bi. Agnes Kisaka Meena, amesema Bandari ya Uvuvi ya Kilwa Masoko ni miongoni mwa miradi muhimu inayolenga kuongeza uzalishaji, uchakataji na thamani ya mazao ya uvuvi nchini.
Amefafanua kuwa lengo kuu la ujenzi wa bandari hiyo ni kuimarisha mnyororo wa thamani wa mazao ya uvuvi kwa kuwezesha uhifadhi bora, uchakataji wa kisasa na upatikanaji wa masoko yenye tija zaidi.
Naye Mkurugenzi wa Uendelezaji wa Miundombinu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Mhandisi George Kwandu, amesema matokeo ya majaribio yanaonesha kuwa mitambo yote inafanya kazi kwa ufanisi mkubwa na kukidhi viwango vilivyokusudiwa.
Amesema mradi huo unatarajiwa kukamilika baada ya Majaribio ya Mitambo na Miundombinu mbalimbali ya Bandari hiyo, kabla ya kuanza kutoa huduma kwa wananchi na wadau wa sekta ya uvuvi.












