* FETA yatakiwa kuongeza kasi ya uzalishaji vifaranga vya samaki, kutoka 450,000 kwa mwezi hadi angalau milioni 10
* Taasisi (FETA) kujenga Meli maalumu ya mafunzo yenye thamani ya dola za Kimatekani milioni 8.3.
DODOMA: SERIKALI imeiagiza Wakala wa Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA) kuharakisha mchakato wa kutoa mafunzo ya viwango vya kimataifa vya usimamizi wa meli na uvuvi katika bahari kuu, (STCW-F).
Mafunzo hayo ambayo yatatolewa kwa mara ya kwanza nchini Tanzania yanatarajia kuimarisha ufanisi wa sekta ya uvuvi na kuchochea uchumi wa buluu.
Naibu Waziri wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bi. Ng’wasi Damas Kamani, alisema Serikali kupitia Wizara mama inatekeleza mkakati endelevu wa kukuza sekta ya uvuvi nchini Ili kukuza uchumi na kufungua ajira zaidi, hasa kwa vijana.
Waziri Kamani alitoa maagizo hayo Jijini Dodoma wakati wa ghalfa maalumu ya uzinduzi wa bodi ya tatu ya ushauri ya FETA.
Viwango vya STCW-F ni kanuni zinazotambulika kimataifa zinazohakikisha wafanyikazi wa majini wana ujuzi na ustadi unaohitajika kufanya kazi kwa usahihi baharini.
“Kuanzisha programu hizi mbili za mafunzo kutasaidia kuzalisha wataalamu wenye ujuzi wa viwango vinavyopendekezwa kimataifa katika uvuvi wa bahari kuu," alisema.
Aidha, alisisitiza Bodi kujikita katika kukuza matumizi ya teknolojia za kisasa za uvuvi Ili kuhakikisha sekta hiyo inazidi kukua kulingana na kasi kubwa ya mabadiliko ya teknolojia duniani.
Alibainisha kuwa, Tanzania inakosa fursa za kiuchumi ya kuvua katika bahari kuu kutokana na changamoto mbalimbali, kama miundombinu duni ya kiteknolojia, pamoja na upungufu wa wataalamu wenye ujuzi wa teknolojia za kisasa.
Waziri Kamani pia aliiagiza FETA kuongeza uzalishaji wa vifaranga vya samaki, kutoka 450,000 kwa mwezi hadi angalau milioni 10, huku akisisitiza kuimarishwa ubora wa mbegu zinazozalishwa.
Zaidi ya hayo, aliipa Bodi jukumu la kusimamia kwa uangalifu matumizi ya ardhi ya wakala huo.
"Serikali inatekeleza Mpango maalumu wa kuwashirikisha vijana katika sekta ya uvuvi kupitia programu ya Building Better Tomorrow (BBT), na hivi karibuni tunaenda kutoa fedha kwa vijana wanufaika Ili kuwawezesha kuanza miradi," alisema.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu waWizara ya Uvuvi, Bi. Agnes Meena alieleza kuwa na imani na utendaji wa wajumbe wapya wa Bodi hiyo, akiwaelezea kuwa na uzoefu na wenye kuzingatia matokeo chanya.
Aliwataka kuhakikisha Bodi hiyo inatekeleza afua za kuboresha na kuendeleza rasilimali ya samaki nchini.
Mtendaji Mkuu wa FETA, Dk. Semvua Mzighani, alisema kuwa maandalizi ya kutoa kozi hizo mbili yanaendelea vizuri.
Ili kuhakikisha mafunzo ya vitendo, alisema wakala unajenga meli maalumu ya mafunzo yenye thamani ya dola za Kimatekani milioni 8.3.
“Ununuzi wa vifaa vya meli unaendelea vyema, na chombo hiki kitakuwa muhimu katika kuwapa wanafunzi ujuzi kwa vitendo,” alisema.
Alisisitiza kuwa, FETA yenye vyuo vitano vya kutoka mafunzo ya uvuvi, itaendelea kujikita katika utoaji wa mafunzo ya uweledi wa teknolojia za kisasa za uvuvi na usimamizi wa bahari ii kuhakikisha sekta inakuwa kwa kasi nchini.
" Dira yetu ni kuhakikisha Taasisi inaendelea kuwa kitovu cha umahiri katika elimu na mafunzo ya uvuvi na ufugaji viumbe maji katika Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara, kwa kuendeleza uvuvi endelevu, ufugaji viumbe maji, na utafiti wa rasilimali za maji, sambamba na kuhamasisha ubunifu na ushirikishwaji wa maarifa katika sekta hii,"
"Kwa sasa, tunaendelea kuhuisha mitaala mipya 12 ili kuendana na mahitaji ya sasa ya soko," alibainisha.
Mwenye kiti cha Bodi hiyo, Dkt. Blandina Lugendo, alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa mchango wake mkubwa kwa maendeleo ya uvuvi na kuahidi kuwa bodi hiyo itatekeleza kwa bidii maagizo ya serikali.
Changamoto hizo ni pamoja na uchache wa manokofu barafu ya kuhifadhia samaki, miundombinu duni, hasa kwa wavuvi wadogo.
KUHUSU FETA
Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA) ni taasisi ya serikali nchini Tanzania chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi, inayohusika na kutoa mafunzo ya elimu ya uvuvi, ufugaji wa samaki, na teknolojia zinazohusiana.
FETA inalenga kuendeleza sekta ya uvuvi kwa kutoa mafunzo, kufanya tafiti, kuzalisha vifaranga, na kutoa ushauri wa kitaalamu.
MJUKUMU YA FETA:
Mafunzo: Kutoa elimu ya sayansi ya uvuvi, ufugaji wa samaki, na usimamizi wa rasilimali za majini.
Tafiti na Ubunifu: Kufanya tafiti shirikishi na kusambaza teknolojia mpya za uvuvi.
Uzalishaji: Kuzalisha samaki, vifaranga, na chakula cha samaki.
Ushauri na Huduma: Kutoa ushauri wa ugani, kutengeneza boti za uvuvi, na nyavu.
Kukuza Biashara: Kuendeleza biashara ya samaki na ufugaji wa viumbe maji.
FETA ina kampasi mbalimbali nchini, ikiwa ni pamoja na Nyegezi-Mwanza, na ina mipango ya kujenga chuo cha kimataifa cha uvuvi Bagamoyo.









Post a Comment